Advertisement |
Jamal Malinzi,Rais wa TFF. PICHA|MAKTABA
Tangu Ligi Kuu ya Tanzania Bara ianze Septemba mwaka jana,
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likiipangua ratiba yake kwa
sababu mbalimbali.
Sababu hizo ni viwanja wanavyokuwa wamepanga
kuvitumia kwa ajili ya ligi hiyo kuhitajika kwa shughuli nyingine za
kisiasa, maandalizi ya timu ya Taifa, maombi binafsi ya dharura ya timu
hivyo kubadilisha tarehe ya mechi na Kombe la Mapinduzi.
Kutokana na sababu hizo, TFF imekuwa ikilazimika kujikuta mara kwa mara ikibadilisha ratiba yake ya Ligi Kuu.
Mabadiliko hayo ni kama maji yaliyokwisha
kumwagika kwani yameshafanyika na ligi inaendelea. Lakini yameacha
athari kubwa na ndiyo maana tunataka suala la mabadiliko ya ratiba
lishughulikiwe haraka na TFF ili kulipunguza au kulimaliza kabisa.
Inafahamika wazi kwamba kabla ya ligi kuanza, TFF
hupata nafasi ya kuandaa kalenda yake ya matukio ya mwaka mzima na
kuipeleka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na vyama vya soka vya mikoani
kufahamu kalenda hiyo.
Vyama vya soka mikoani ndiyo vinavyofanya kazi ya
kuomba matumizi ya viwanja husika mikoani hivyo kama TFF ilipanga ratiba
yake ya matukio msimu huu bila kuangalia ratiba za shughuli kubwa za
kisiasa za nchi, matamasha mbalimbali na shughuli nyingine za michezo,
lazima hilo litawapa tabu viongozi wa vyama vya soka mikoani.
Upangaji wa ratiba ya ligi kubwa na muhimu kama
hiyo unahitaji umakini wa hali ya juu. Haipendezi hata kidogo kuona kila
mara inafanyiwa marekebisho. Tungependa kuona ratiba ambayo angalau
inatekelezeka kwa asilimia zaidi ya 80 bila kufanyiwa marekebisho.
Tunasema walau kwa asilimia 80 tukitilia maanani
ugumu uliokuwapo katika upangaji ratiba kwani ni dhahiri kwamba
miundombinu yetu ya nchi na matukio mengine, hayawezi kukwepeka.
Lakini suala kama ratiba ya ligi kuingiliwa na
mechi za kimataifa ni uzembe kwa kuwa siyo mambo yanayozuka ghafla.
Mechi hizo au tarehe zake zinafahamika vyema ni suala la umakini tu.
Mbali na hilo, jambo jingine linalotushangaza ni
kuona kwamba yanapofanyika marekebisho ya ratiba yanatolewa bila
kuonyesha mabadiliko yaliyofanyika na ratiba mpya itakavyokuwa.
Hivi sasa tumekuwa tukitumiwa barua pepe na Ofisa
Habari wa TFF kwamba mechi za wiki hii za Ligi Kuu ya Vodacom ni kama
ifuatavyo; Februari 21- Mbeya City vs Yanga, Kagera Sugar vs JKT
Ruvu, Mgambo Shooting vs Mtibwa Sugar, Feb 22- Stand United vs Simba,
Azam vs Tanzania Prisons. Februari 25- Mbeya City vs Ruvu Shooting.
Tunaamini kwamba kama TFF ingekuwa makini katika
suala hili la Katiba, mosi isingeruhusu kuwa na viraka vingi, lakini
pili ingekuwa na mabadiliko machache ambayo yangetoa fursa kwa wadau
kuyafahamu kirahisi na kujipanga kwa maana ya timu kujiandaa na
mashabiki pia.
Tunasema hivyo kwa sababu hivi sasa ni rahisi kuwa na ratiba
sahihi ya Ligi ya England, Ujerumani, Italia na Hispania kuliko kuwa na
ratiba sahihi ya mechi zijazo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Tunaamini kuwa mashabiki wa soka wa Tanzania
wanapenda kuona ratiba sahihi ya mechi zijazo za Ligi Kuu ya Tanzania
Bara na takwimu nyingi zinazohusu ligi hiyo.
Tunatarajia TFF itatoa ratiba mpya na kupunguza
kutengeneza ratiba ambayo itakuwa inapanguliwa mara kwa mara ili ligi
hiyo siyo tu kwamba isikose mvuto, bali kuepuka kero na aibu hii.
0 Post a Comment: